Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Habari

Waziri Kalemani aiagiza PURA kuongeza nguvu shughuli za utafutaji mafuta na gesi asiliaNa JANETH MESOMAPYA

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amekutana na kufanya mazungumzo na Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA). Waziri Kalemani alikuwa akifunga mafunzo maalumu yaliyotolewa kwa Bodi hiyo mjini Tanga.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha Waziri, Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Gasper Mhinzi ameeleza kuwa wamejipanga kuhakikisha kuwa PURA inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Petroli katika kuiletea tija sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini.

Katika mazungumzo yake na Bodi hiyo, Waziri Kalemani ameipongeza Bodi kwa kazi nzuri inayoifanya ya kuisimamia PURA na kuhakikisha inafanya kazi kwa weledi na ufanisi licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali za rasilimali watu na nyinginezo.

Sambamba na hilo, ameiagiza Bodi hiyo kuhakikisha PURA inaongeza nguvu katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

“Tuweke nguvu ili tugundue mafuta, Watanzania wanataka mafuta,” aliongeza.

Waziri Kalemani pia ameiagiza Bodi na Menejimenti kuimarisha usimamizi wa ushirikishwaji wa wazawa kwenye shughuli za mkondo wa juu wa petroli kwa kuzingatia Kanuni za Ushirikishwaji wa Wazawa katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia.

Aidha, amehitimisha mafunzo hayo na kuwasihi wamufaika wake hao, kuhakikisha wanatumia elimu waliyoipata kuboresha utendaji wao huku akisisitiza “masuala mliyojifunza ni muhimu sana katika kufahamu mwelekeo wa sekta pamoja na mwelekeo wa serikali.”

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bi. Beng’i Issa amemshukuru Waziri kwa kuhitimisha mafunzo hayo na kumuahidi kwa niaba ya Bodi, kufanyia kazi maagizo yote aliyoyatoa katika kuiongezea tija sekta ya mafuta na gesi asilia.