Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Habari

Menejimenti, Watumishi PURA waaswa kufanya kazi kwa weledi, bidii


Na JANETH MESOMAPYA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Leonard Masanja, Jumatatu Oktoba 26, 2020 alitembelea ofisi za Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu Petroli (PURA) jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo Mhandisi Masanja alifanya mazungumzo na Menejimenti na wafanyakazi wa PURA na kutoa rai kwao kufanya kazi kwa bidii na weledi kwa manufaa ya taifa.

Licha ya Mamlaka hiyo kuwa changa, na kukabiliana na changamoto mbalimbali kama uchache wa watumishi huku wengi wao wakikaimu nafasi mbalimbali za uongozi, Mhandisi Masanja aliwaeleza watumishi hao kuwa ni muhimu kuzitumikia nafasi hizo kwa ufanisi na ubunifu mkubwa.

“Viongozi mnaokaimu nafasi mbalimbali za uongozi, hii ni fursa kwenu kufanya kazi kwa bidii na kuuonyesha umma wa Watanzania uwezo wenu wa kuongoza Mamlaka hii ambayo ilianzishwa kwa kuzingatia maslahi mapana ya taifa letu kupitia sekta ya mafuta na gesi,” alisema.

Akizungumzia hali ya mafuta na gesi nchini, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA Mhandisi Charles Sangweni alieleza kuwa hadi sasa kiasi cha gesi kilichogundulika ni futi za ujazo trilioni 57.54.

“Kati ya kiasi hiki kilichopatikana, gesi iliyogundulika nchi kavu ni futi za ujazo trilioni 10.41 huku iliyogundulika Bahari Kuu ni futi za ujazo trilioni 47.13,” aliongeza.

Katika ziara hiyo Mhandisi Masanja aliongozana na viongozi wa Wizara ya Nishati, akiwepo Kamishna wa Petroli na Gesi, Adam Zuber, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Raphael Nombo na makamishna wasaidizi kutoka idara ya Mafuta na Gesi.