Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Habari

Wito watolewa, fursa za mradi wa bomba EACOPNa Janeth Mesomapya

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ametoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa zinazoambatana na utekelezwaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi Chongoleani Tanga (EACOP).

Ametoa wito hiyo leo, Julai 3, 2021 kwenye semina ya wadau wa sekta binafsi kuhusu fursa zinazopatikana kwenye mradi huo wa EACOP. Semina hiyo imeratibiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na kufanyika mjini Tanga.

“Mradi huu ni muhimu sana kwa wadau wa sekta binafsi nchini, mna haki ya kutumia fursa zinazotokana na mradi huu lakini pia mna wajibu wa kutekeleza fursa hizo kwa weledi na ufanisi mkubwa,” alisema.

Akizungumza kuhusu ushirikishwaji wa wazawa kwenye utekelezwaji wa mradi huo, Waziri Kalemani ameiagiza kampuni ya EACOP kuhakikisha inatumia huduma na bidhaa zinazozalishwa nchini katika utekelezwaji wa mradi husika, isipokuwa kwa bidhaa na huduma zenye ulazima wa kupatikana nje ya nchi.

“EACOP hakikisheni vifaa vyote vya ujenzi wa bomba vinatokea nchini ikiwa ni pamoja na mabomba ya kupitisha mafuta, nawasihi Watanzania wenye utayari wa kuanzisha viwanda vya kutengeneza mabomba, chukueni mikopo kwenye mabenki na muanze uzalishaji ili bidhaa hizo zipatikane kirahisi,” alisisitiza.

Vivyo hivyo Waziri Kalemani ameiagiza TPDC kuhakikisha Watanzania wanapata kipaumbele kwenye nafasi za ajira, hususani ambazo ni nyeti na zenye thamani kubwa.

“Kuna nafasi za ajira takriban 15,000 kwenye utekelezwaji wa mradi huu, naagiza nafasi hizi zitolewe kwa Watanzania hususani wa kada rasmi na sio tu wafanyabiashara wadogo, wafanya usafi na kadhalika,” aliongeza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC James Mataragio, alieleza kuwa baadhi ya fursa zilizopo kwenye utekelezwaji wa mradi huo ni pamoja na huduma za kandarasi, vifaa vya ujenzi, usafirishaji, vyakula na vinywaji, hoteli na upishi, bidhaa za mafuta, vifaa vya ofisi na nyinginezo.

Imeelezwa kuwa mradi huu ni wa thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.5 na utapita kwenye mikoa 8 ya Tanzania bara huku ukitarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 36.