Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Habari

Wafanyakazi PURA wapatiwa mfunzo ya maadili, rushwa, UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza


Na Ebeneza Mollel

Katika kutekeleza malengo ya Serikali ya kuendelea kupambana na rushwa na kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI na magonjwa sugu yasivyoambukiza, Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli imefanya semina ya siku moja kwa watumishi wake yenye lengo la kuongeza uelewa kwenye maeneo husika.

Semina hiyo ilifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa PURA jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi na wafanyakazi wa taasisi hiyo. Watoa mada katika semina walikuwa maafisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupamabana na Rushwa (TAKUKURU) na Tume ya Taifa ya Kupambana na Ukimwi (TACAIDS).

Akizungumza katika ufunguzi wa semina hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni alisema mafunzo hayo ni muhimu sana kwani yataongeza uelewa wa watumishi wa taasisi hiyo katika maeneo ya maadili, rushwa na UKIMWI hivyo kuwasaidia kufanya kazi kwa uadilifu zaidi huku wakizitunza afya zao na jamii kwa ujumla.

Akiwasilisha mada ya maadili katika semina hiyo, Afisa Mwandamizi kutoka TAKUKURU, Bi. Marcella Salu alieleza kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya maadili na rushwa ndio maana ni muhimu kuzungumzia masuala hayo kwa pamoja akisisitiza "kufanya kazi kwa uadilifu, kutoa huduma bila upendeleo na ufahamu wa sheria ni masuala ya msingi kuzingatiwa katika utendaji kazi".

Naye, Bi. Elly Makala wa TAKUKURU alizungumzia makosa ya rushwa kama yalivyotajwa katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007 na kuongeza kuwa rushwa husababishwa na mambo mbalimbali yakiwemo mmomonyoko wa maadili, tamaa, ubinafisi, kutokufahamu haki na wajibu, mitindo ya maisha, na upungufu wa wafanyakazi pamoja na vitendea kazi.

Kwa upande wake, Dkt. Patric Kanyamwenge kutoka TACAIDS alizungumzia masuala ya dhana nzima ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI, aina ya virusi vya UKIMWI, njia za maambukizi ya virusi vya UKIMWI, na matumizi ya dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARV).

Aidha, mwezeshaji huyo alieleza hali ya maambukizi nchini na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kupambana na virusi ya UKIMWI na UKIMWI. Vile vile, Mwezeshaji huyo alieleza kuwa mpango wa Serikali katika suala la kupambana na virusi vya UKIMWI na UKIMWI ni kufikia sifuri tatu (000) ifikapo mwaka 2030 kwa maana ya maambukizi sifuri (0), unyanyapaa sifuri(0) na vifo sifuri(0).

Kwa upande wa Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza, Dkt. Hafidh Ameir kutoka TACAIDS alieleza namna mazoezi, ulaji wa chakula bora, unywaji maji na uthibiti wa msongo wa mawazo vinavyoweza kumuepusha mtu dhidi ya magonjwa sugu yasiyoambukiza.

Katika kuhitimisha semina hiyo, Afisa Rasilimaliwatu kutoka PURA, Bi. Sabrina Seif alieleza kuwa PURA itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kutimiza malengo ya Serikali dhidi ya UKIMWI, Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza pamoja na Rushwa huku akiwasihi watumishi wa PURA kuweka katika matendo yale yaliyofundishwa katika semina hiyo.

Sambamba na semina hiyo, watumishi wa PURA walioshiriki mafunzo walipata fursa ya kupima afya zao ambapo walipata kupima magonjwa ya kuambukiza kama vile virusi vya UKIMWI na magonjwa yasiyo ya kumbukiza yakiwemo kisukari na shinikizo la damu.