Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Karibu

Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) ninayo furaha kuwakaribisha kwenye tovuti yetu ambayo imeboreshwa kwa lengo la kuhabarisha umma kuhusu shughuli zinazofanywa na Mamlaka hii.

Katika kuzingatia umuhimu wa sekta ya mafuta na gesi nchini, PURA imejidhatiti kuendelea kutimiza majukumu yake iliyopewa kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015.

Majukumu hayo ni pamoja na kuishauri Serikali juu ya masuala yanayohusu Mkondo wa Juu wa Petroli katika utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini, kusimamia na kudhibiti shughuli za Mkondo wa Juu wa Petroli na kusimamia shughuli zote za mradi wa kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG).

Katika kutimiza majukumu haya, PURA itaendelea kutengeneza mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji kwa kuzingatia itikadi ya chama tawala na adhma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kufikia uchumi wa viwanda pamoja na kuhakikisha ushiriki wa wazawa katika Shughuli za Mkondo wa Juu wa Petroli unaongezeka.

Ushiriki wa wazawa katika uwekezaji wa sekta hii ni nyezo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa taifa kwani hupelekea ongezeko la ajira, kuhamishwa kwa teknolojia na kuongeza thamani kwenye bidhaa na huduma zinazozalishwa na zinazotolewa ndani ya nchi.

Ni imani yangu kuwa tovuti hii itasaidia sana kuonyesha kwa uwazi shughuli hizi zinazofanywa na Mamlaka hii kwa umma wa Watanzania ikiwa ni pamoja na kuongeza uelewa wa masuala yote yanayohusu sekta ya mafuta na gesi nchini Tanzania.

Tunashukuru kwa ushirikiano wenu na karibuni sana.

Mha. Charles Sangweni

Kaimu Mkurugenzi Mkuu