Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Habari

Wanagenzi PURA watembelea maeneo ya kijiolojia, mitambo ya uzalishaji gesi asilia


Na JANETH MESOMAPYA

Timu ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) hivi karibuni wameongoza jopo la wanafunzi wa mafunzo kwa vitendo (interns & field students) kwenye Mamlaka hiyo kutembelea miradi na mitambo mbalimbali ya uzalishaji na uchakataji wa gesi asilia mkoani Mtwara na Lindi.

Katika ziara hiyo wanafunzi hao wamepata fursa ya kutembelea mradi wa kupokea gesi asilia Kinyerezi (GRF), Kisima cha Mkuranga 1, eneo la uzalishaji gesi asilia Mnazi Bay, mitambo ya kuchakata gesi asilia Madimba na mitambo ya kupokea gesi Mtwara.

Jopo hilo pia lilitembelea maeneo ya kijiolojia (geological sites) sita na maeneo mawili yenye mvujo wa mafuta (oil seep) ya Wingayongo na Makukwa.

Kwa mujibu wa kiongozi wa ziara hiyo, Mjiolojia Faustine Matiku ziara hiyo ilikuwa na lengo law kuwaonyesha kwa vitendo wanafunzi hao kazi ambazo PURA inafanya na miradi ambayo inaidhibiti kwa mujibu wa sheria.

“Timu hii ilikuwa pia na wanafunzi wasio na taaluma za jiolojia na uhandisi wa petroli hii ilikuwa ni kuwawezesha kupata uelewa wa shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia,” alieleza.

Akizungumzia maeneo ya kijiolojia yaliyotembelewa, Mjiolojia wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) Adam Sajilo ameeleza kuwa wanafunzi hao wameona miamba inayopatikana kwenye pwani ya kusini mwa Tanzania na kujifunza aina zake na jinsi ilivyotengenezwa.

“Wameweza hata kujifunza kuwa hata miamba ina umri na unaweza kujua umri wa mwamba fulani kwa kuangalia viumbe walio kwenye mwamba husika,” aliongeza.

Mwanagenzi Mjiolojia Bahati Mohamed ameeleza kuwa ziara hiyo imekuwa ya manufaa kwake kwani amefanikiwa kuona kwa macho vitu ambavyo vinatengeneza rasilimali za mafuta na gesi ardhini.

Kwa upande wake, Naomi Mwakibolwa ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa nne wa Shahada ya Uhandisi wa Petroli katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ameeleza kuwa ziara hiyo imemsaidia kuhusianisha vitu alivyofundishwa darasani na uhalisia wake kiutendaji kwenye maeneo ya uzalishaji.

Naye Mwanagenzi wa kada ya Manunuzi Winston Kayona amesema ziara hiyo imemsaidia kujifunza umuhimu wa mchakato wa manunuzi katika kuleta maendeleo kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya mafuta na gesi.