Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Habari

PURA, wajumbe wizara ya nishati watembelea miradi ya gesi asilia Mtwara


Na JANETH MESOMAPYA

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi Charles Sangweni hivi karibuni aliongoza wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi wa Ndani wa Wizara ya Nishati kufanya ziara kwenye visima na mitambo ya uzalishaji wa gesi asilia mkoani Mtwara.

Mhandisi Sangweni alieleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kujenga uelewa kwa wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi wa Ndani ya Wizara na sekretarieti yake juu ya shughuli za Mkondo wa Juu wa Petroli ikiwemo uzalishaji wa gesi asilia ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Ujumbe huo ulitembelea kitalu cha uzalishaji wa gesi asilia cha Mnazi Bay kinachoendeshwa na Kampuni ya Maurel & Prom (M&P). Katika kitalu hicho maeneo yaliyotembelewa ni mitambo wa kuchakata gesi asilia (Gas Processing Facility), visima vya uzalishaji pamoja na mitambo wa kupokea gesi asilia (Gas Receiving Facility).

Ziara hiyo iliendelea hadi kwenye mitambo ya kuchakata gesi asilia ya Madimba (Madimba Processing Plant) iliyo chini ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na baadaye kutembelea mitambo ya kupokea gesi asilia kutoka Mtwara na Songosongo (Somangafungu Gas Junction).

Mitambo hii ya Somangafungu ambayo pia iko chini ya TPDC huisafisha zaidi gesi iliyopokelewa na baadaye kuisafirisha hadi kwenye mitambo ya kupokea gesi asilia ya Kinyerezi jijini Dar es Salaam (Kinyerezi Gas Receiving Station).