Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Habari

PURA yashiriki kwenye Maonesho ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Arusha


Timu ya Wataalamu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) wameshiriki kwenye Maonesho ya Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, katika viwanja vya Sheikh Amri Abed, jijini Arusha.

Maonesho hayo yameandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), ambayo yameanza rasmi, Jumapili, Februari 7, 2021 hadi Jumamosi, Februari 13, 2021.

Mgeni Rasmi, Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa, atayafungua rasmi maonesho haya Februari 9, 2021 huku yakitarajiwa kufungwa na Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu Mh. Jenista Mhagama Februari 13, 2021.

Baadhi ya masuala ambayo wataalamu wa PURA wanayazungumza na kuyatolea ufafanuzi kwenye banda la PURA namba 27, ni pamoja na uanzishwaji wa PURA, majukumu yake, shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia, fursa zilizopo na Ushiriki wa wazawa katika sekta ya Mafuta na Gesi na mengineyo.

Madhumuni ya maonesho haya ni kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu uwepo, majukumu na vigezo vinavyotumika katika kutoa huduma za mifuko ya uwezeshaji ili kuwafahamasisha wananchi kunufaika na fursa zilizopo katika mifuko hiyo.

Vilevile dhumuni lingine ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza katika miradi mbalimbali yenye kuleta faida kupitia uanzishwaji na uimarishwaji wa vikundi vya kifedha vya kijamii.