Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli

Habari

PURA, wadau kuongeza ushiriki wa wazawa sekta ya mafuta na gesi


Na JANETH MESOMAPYA

Katika kuhakikisha ongezeko la ushiriki wa Watanzania katika shughuli za mkondo wa juu wa Petroli, Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imekutana na wadau wa sekta ya mafuta na gesi kujadili jinsi bora ya kufanikisha suala hilo.

Katika kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA Mhandisi Charles Sangweni ameeleza kuwa moja ya majukumu ya Mamlaka hiyo ni kuhakikisha wazawa wanashiriki kikamilifu kwenye sekta ya mafuta na gesi kwa kuuza bidhaa na kutoa huduma pamoja kupata nafasi za ajira.

Aliongeza kuwa kufanikiwa kwa jukumu hilo kutategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano baina ya Mamlaka na wawekezaji wa sekta hiyo pamoja na wadau hao kufuata sheria na miongozo inayoelekeza jinsi ya Watanzania kushiriki katika sekta hiyo

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ushiriki wa Wazawa (Local Content & Stakeholders Engagement) Charles Nyangi alieleza kuwa lengo kuu la kikao hicho ni kuandaa vigezo ambavyo vitawezesha Watanzania kuuza bidhaa na kutoa huduma zenye ubora ili kukidhi mahitaji ya soko.

Alidokeza kuwa kwasasa PURA ikishirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) zinaandaa kanzidata (database) ambayo itatunza taarifa zote muhimu za Watanzania wanaotaka kushiriki kwenye sekta hiyo kwa kuuza bidhaa, kutoa huduma au kupata nafasi za ajira.

“Lengo la kanzidata hii ni kuwa jukwaa la kukutanisha Watanzania watoa huduma na makampuni ya kimataifa ya mafuta na gesi yanayofanya uwekezaji nchini ambayo yanauhitaji wa bidhaa na huduma mbalimbali ambazo zinaweza kupatikana ndani ya nchi,” alisema

Nao wadau walioshiriki kikao hicho walitoa rai kwa Mamlaka kuhakikisha inaendelea kutoa elimu ya kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kutumia fursa zilizopo kwenye tasnia hiyo kwa kuuza bidhaa na kutoa huduma bora na kuwapiku washindani wao wa nje ya nchi ili kujiongezea tija kiuchumi.